SASA MWANZA NI KILA KITU

SASA MWANZA NI KILA KITU

KARIBU KISIWA CHA RUBONDO

KARIBU KISIWA CHA RUBONDO

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, March 21, 2018

RAIS WA MYNMAR AJIUZULU.


Rais wa Myanmar Htin Kyaw amejiuzulu, kulingana na afisi yake.

Hakuna sababu ilitolewa lakini kumekuwa na wasiwasi katika miezi ya hivi karibuni kuhusu afya ya rais huyo mwenye umri wa miaka 71 baada ya kuonekana amedhoofika katika hafla moja.

Htin Kyaw alliapishwa kuwa rais 2016 baada ya uchaguzi uliositisha miongo kadhaa ya uongozi wa kijeshi.

Lakini alikuwa kiongozi asiye na mamlaka huku aliyekuwa kiongozi wa upinzani wa muda mrefu Aung San Suu Kyi akiwa kiongozi mwenye mamlaka.

Taarifa iliochapishwa katika mtandao wa facebook wa rais huyo ilisema kuwa Htin alitaka kupumzika.

Makamu wa rais Myint Swe , jenerali wa zamani atakuwa kaimu rais hadi pale rais mpya atakapochaguliwa katika muda wa siku saba sijazo, taarifa hiyo ilisema.

Bi Suu Kyi, ambaye alifungwa kwa miaka kadhaa chini ya uongozi wa kijeshi wa Junta alipigwa marufuku kuchukua wadhfa huo.

Kipengee cha katiba kilichotengezwa ili kuhakikisha achukui wadhfa huo kinasema kuwa hakuna raia mwenye watoto kutoka nje anaweza kuwa rais.

Alikuwa na watoto wawili na mumewe raia wa Uingereza.

Htin Kyaw alikuwa rafikiye wa utotoni na mshauri wake wa zamnai na wakati mwengine dereva. Alionekana kuwa mtulivu na mtu alimuamini sana.

HATIMAYE ABDUL NONDO AMEFIKISHWA MAHAKAMANI MKOANI IRINGA

Hatimaye Abdul Nondo amefikishwa Mahakamani Iringa Tanzania
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo amesafirishwa usiku wa kuamkia leo Machi 21, 2018 kupelekwa mkoani Iringa.
Taarifa zilizotolewa na wakili wake, Jebra Kambole leo Jumatano zinaeleza kuwa sasa Nondo yupo Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa.
Nondo anadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Machi 6, 2018 na siku inayofuata akaonekana mjini Mafinga, wilayani Mufindi, Iringa ambako alishikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo na baadaye kurejeshwa Dar es Salaam.
Tangu akamatwe Nondo hajawahi kuzungumza na wakili wake wala mtu yeyote wa karibu yake jambo ambalo limekuwa likipingwa na watetezi wa haki za binadamu.
Jana, Jebra alisema kuwa wamefungua kesi ya kuiomba mahakama kumpa dhamana Nondo, kutoa amri ya kuwapa mawakili haki ya kuonana naye na kuitaka mahakama itamke mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) ameshtakiwa kinyume cha sheria.
Kumekuwepo kesi kadhaa za kutoweka watu hususan wanasiasa nchini Tanzania suala ambalo limezusha wasiwasi kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama nchini humo.

BARUA YA WAZI KWA NAIBU WAZIRI WA HABARI UTAMADUNI VIJANA NA MICHEZO KUTOKA WASAFI.


Muheshimiwa Salaam,
Natumai u mzima wa afya.

Najua una nia nzuri ya kulinda maadili y amwafrika na hasa ya mtanzania na kuhakikisha basi hakuna ovu lolote linaloweza kuichafua sifa yetu lakini kubwa jamii zetu. Ila naomba nisahihishe approach yako.

Muheshimiwa kuna vitu vinaitwa Ratings nadhani huu ni Muda muafaka kwa tasnia yetu kuanza kua na hii system ili basi wasanii wafanye kazi kwa uhuru na pia hadhira (watazamaji na waskilizaji) pia wasipitwe ama kukosa kazi za wasanii wanaowapenda
Mfano wa ratings ni G ikiwa inamaanisha General yaani yeyote anaweza kutazama
PG hii inaweza tazamwa na yeyote ila watoto wanahitaji usimamizi wa wazazi kwani kuna baadhi ya material sio kwa ajili yao PG-13 wazazi wanahitajika, ikiwezekana aitazame movie, video yote kwanza kabla ya kumuonesha mtoto Na zingine kibao.
Hii ni 2018 sio mwaka 1903 sasa ivi tunachotakiwa kufanya ni kuanza kutambulisha hii system na sio kufungia nyimbo. 

Lakini mbali na hayo, badala ya kushusha na kuzuia wasaniii kama kina @diamondplatnumz na wengine mlofungia kazi zao embu tazameni Tasnia nzima kwa ujumla. 

Kuna watu wanatamani sana kuingia katika sanaa wakiwa na vipaji na uwezo ila wakiangalia yanayowakuta malegend kama kina majuto wanakata tamaa. Huwezi nambia mzee kama majuto leo na movie zote alizoekt hakuna kitu tasnia imeweza kumfanyia na yeye aishi kama hadhi ya jina lake.

Si majuto tuu wako wasanii wengi sana ambao wananafasi kubwa katika kuelimisha jamii lakini maisha wanayoishi ni tofauti na status zao. Je sanaa sasa ni kulinda maadili tu ama ni ajira pia? 

Kazi za wasanii zinasimamiwa ipasavyo?

Je! Mnahakikisha kwamba wasanii hawanyonywi na mapromota?
Mnahakikisha kwamba hakuna watu ambao wao ndo wanajifanya Miungu wa kuwatawala wasanii na kuwanyonya wanaokataa kuwaabudu?

Ama wewe unaona kuzuia kazi ndo la msingi?

Unajua kwamba @diamondplatnumz ni msanii wa kimataifa kutoka Tanzania? 

Unataka afate maadili ya kitanzania Jeh! Mashabiki zake wa nje nao kama wamarekani wanaishi maadili ya kitanzania? Kiti umepewa sio ulemaze sanaa yetu irudi nyuma, ivushe ifike mbali. 

Badili sana yetu iwe accessible kimataifa sio kuiwekea mipaka.

Ni hayo tu Muheshimiwa naibu Waziri
Salaam kwako.

Tuesday, March 20, 2018

MNEC MWAKA RAMADHAN AMEVUNA WANACHAMA WAPYA (80) KATA YA MKWAWA MANISPAA YA IRINGA

 Mjumbe wa halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi (CCM) Taifa na mjumbe wa kamati utekelezaji wa UWT taifa Mwaka Ramadhan akiongea na wanawake waliokuwa wamejitokeza kumsikiliza kwenye ziara ya UWT taifa mkoani Iringa katika Kata ya Mkwawa
Baadhi ya wanachama waliojiunga na umoja wa wanawake UWT katika kata ya Mkwawa wakatika wa ziara ya viongozi wa kitaifa mkoani Iringa
Baadhi ya wanachama wa chama cha mapinduzi wakiwa katika kitendo cha kula kiapo pamoja na wanachama waliojiunga na umoja wa wanawake UWT kata ya Mkwawa
 Mjumbe wa halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi (CCM) Taifa na mjumbe wa kamati utekelezaji wa UWT taifa Mwaka Ramadhan akiwa na mbunge wa viti maalum Ritta Kabati pamoja na mwenyekiti wa UWT manispaa ya Iringa Ashura Jongo Pamoja katibu wa UWT manispaa ya Iringa


Na Fredy Mgunda,Iringa

MJUMBE wa halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi (CCM) Taifa na mjumbe wa kamati utekelezaji wa UWT taifa Mwaka Ramadhan amevuna wanachama wapya zaidi ya themanini (80) katika kata ya Mkwawa Manispaa ya Iringa ambo wamejiunga rasmi na umoja huo.

Wanachama hao wamepokelewa wakati wa ziara ya viongozi wa ngazi za juu wa UWT taifa mkoani Iringa, ambapo MNEC Ramadhan alipokuwa akiongea na wanachama pamoja na wananchi wa kata ya Mkwawa ndipo waliposhawishika kujiunga na umoja huo kutokana na hamasa walioipata kutoka kwa MNEC huyo.

Ramadhan alisema kuwa chama cha mapinduzi ni chama ambacho kimejengwa kimisingi ya kulea jumuhia  mbalimbali ambazo zipo ndani ya chama hicho ndio maana bado kinanguvu katika siasa za hapa nchini hata kimekuwa mfano kwa nchi nyingine.

“Jumuiya ya umoja wa wanawake wa chama cha mapinduzi Tanzania ni moja kati ya jumuiya ambayo ipo ndani ya chama hiki na inakazi zake kwa ajili ya kukijenga chama na kuleta maendeleo kwa wananchi waliokipa dhamana ya kuongoza nchi hii” alisema Ramadhan

Aidha Ramadhan aliwataka wanawake kujifunza kujifunza kujitegemea ili waweze kuja kuwaajiri wanaume ambao kwa sasa ndio wamekuwa wakitoa ajira nyingi kwa wanawake hapa nchini.

“Wanawake wenzangu sasa imefika mwisho wa kuwa tegemezi kwa wanaume inatakiwa sasa tusimame sisi kama sisi na tuanze kuwaajiri na kulisha wanaume zenu majumbani kwetu maana tunauwezo wa kufanya kila kazi hizo inatakiwa tujitume” alisema Ramadhan

Ramadhan alisema kuwa wanawake mkiwa mnataka kufanya biashara zenye malengo msiogope kwenda kukopa maana siku hizi kuna mikopo ya bei rahisi na riba yake sio kubwa ambayo itakuwezesha kufanya biashara yako kwa maendeleo yako.

“Siku hizi kuna mabenk mengi yanawakopesha wanawake na wanawaamini sana wanawake kwenye kufanya biasha hivyo nendeni mkakope msiogope maana hizi benk zipo kwa ajiri ya kusaidia kuinua maisha ya mtanzania” alisema Ramadhan

Ramadhan alimalizia kwa kuwataka wanawake wa kata ya Mkwawa mkoani Iringa kuzitumia pesa kwa nidhamu ya hali ya juu ili ziweze kuleta matunda ya kuleta maendeleo ambayo yanahitajika kwa maisha yao.

“Jamani kila pesa ukiitumia kwa nidhamu basi utaona faida yake na itakuletea maendeleo yako na taifa kwa ujumla maana unakuwa umetumia vizuri pesa kwa maendeleo” alisema Ramadhan

Kwa upande wake mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati alisema kuwa atawapatia elimu ya ujasiliamali ili wakipata mitaji waweze kuitumia vizuri kwa ajili ya manufaa ya maendeleo.

“Jamani mimi nimekuwa nikitoa elimu ya ujasiliamali mara kwa mara kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kufanya biashara zenu kwa faida na kutoa elimu ya matumizi ya fedha hivyo nawaomba nikiitisha tena kutoa elimu mkaribia kwa wingi maana huwa inakuwa bure” alisema Kabati

CHAMA CHA USHIRIKA CHA NYANZA KUFUFUKA KWA KASI MONGELA ATANGAZA VITA NA VIONGOZI WAPYA.NA ZEPHANIA MANDIA 
MKUU wa mkoa wa Mwanza John Mongella amewatahadhalisha wajumbe wa zao la pamba kuepuka kuchagua viongozi wasio na sifa kwa kigezo cha kupewa rushwa.

Tahadhali hiyo ameitoa kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Cha Ushirika Nyanza uliofanyika katika ukumbi wa chama hicho katikati ya jiji la Mwanza, huku kukiwa na agenda kadhaa ikiwemo uchaguzi wa viongozi na wajumbe wa bodi ya chama hicho.

"Nasikia wapo tuliowanyang'anya mali za Ushirika walizojimilikisha kwa mlango wa uwani, mara baada ya kujiuzia kwa pesa ndogo, za wizi wizi sasa wamefadhili baadhi ya watu miongoni mwenu kwa kuwapa fedha na nyinyi mnawajua"
 "Wametoa vihela vyao, wamevimwaga kwa wajumbe tunaowaamini na sasa wanataka kurudi kwenye madaraka watusumbue tena"

"Nataka kuwaambia kwamba tunawafahamu wakirudi mtaona, kwani hawatofika hata kesho, tutawafuta"
 WAKATI HUO HUO
Serikali imetakiwa kuendelea kutoa ushirikiano kwenye chama cha Ushirika cha Nyanza na kuweka mikakati thabiti ya kufufua zao la pamba na kulifanya kuwa la biashara ili kuweza kusaidia kendeleza ushirika huo wa Nyanza katika mkoa wa Mwanza.

Chama Cha Ushirika Nyanza kimewakutanisha wanachama wake kutoka mikoa mbalimbali ya Kanda ya Ziwa inayolima zao hilo ambayo ni MWANZA, GEITA NA SIMIYU, lengo kuu likiwa ni kujadili changamoto mbalimbali za zao la pamba na namna ya kuzipatia ufumbuzi.
 Hawa ni baadhi ya washiriki wa mkutano huo kutoka kanda zinazolima zao la pamba nao wanaeleza nini imani yao kwa zao hilo ambalo kwa hivi sasa Serikali imeamua kulisimamia mguu kwa mguu. Akisoma taarifa ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nyanza Simon Mbata ambaye ni mjumbe wa Bodi amewataka viongozi wa Kanda zinazolima zao hilo kuwa waadilifu katika ununuzi 

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella amesema kupitia Nyanza juhudi ziendelee kufanyika hata kulifufua zao hilo.

Kutokana na umaarufu wa zao la pamba wakulima wameamua kulipa jina la dhahabu nyeupe.

Kauli mbiu ya mkutano mkuu wa 26 wa Chama Chama Cha Ushirika Nyanza inasema Tanzania ya Viwanda Itawezekana kupitia vyama vya ushirika vya msingi.

SUGU ATOA RAMBIRAMBI KWA DIWANI WA CCM.

Mhe. Sugu.
Mbunge wa Mbeya mjini kwa tiketi ya (CHADEMA) Joseph Mbilinyi alimaarufu kama Sugu, Jongwe ametoa rambirambi ya laki moja kwenye msiba wa mama mzazi wa Diwani wa Kata ya Ilemi (CCM) Agatha Ngole.

Sugu ambaye amefungwa miezi mitano katika gereza la Rwanda Mbeya kwa kosa la kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais John Magufuli alipata taarifa akiwa gerezani hapo kuwa diwani huyo amefiwa na mama yake mzazi na kuamua kutoa rambirambi ya shilingi laki moja kwa ajili ya msiba huo.

Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga wanatumikia kifungo cha miezi mitano jela katika gereza la Rwanda Mbeya.

CHADEMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini - Nyasa  imethibitisha juu ya taarifa hiyo na kusema ni kweli Sugu ametoa rambirambi hiyo kwa diwani huyo.

MUUNGANO WA MAKANISA KENYA: ASILIMIA KUBWA YA WAKRISTO NI WACHAWI NA WASHIRIKINA.

Muungano wa makanisa nchini Kenya umetangaza kuwa, uchawi na ushirikina umekumbatiwa zaidi na Wakenya, kuliko wanavyomuamini Mungu.
Hayo yamesemwa na Askofu Peter Mburu, mwenyekiti wa muungano huo katika kongamano lililopewa jina la kuombea taifa katika uwanja wa Safaricom Kasarani jijini Nairobi na kuongeza kuwa, uchawi na ushirikina kwa ajili ya kusaka maisha mazuri, utajiri na vyeo, ni mambo ambayo yamekumbatiwa sana na Wakristo. Kwa mujibu wa Askofu Mburu, asilimia kubwa ya wafanyabiashara, wafanyakazi katika nyadhifa tofauti za umma na binafsi, wanasiasa na wengine wengi wameshikamana na uchawi kwa kuutumia kama kinga yao ya maisha.
Wafuasi wa dini ya Kikristo wakiwa kanisani
“Katika muungano wetu tumeweza kuwasimamisha kazi jumla ya wahubiri 23 tangu Januari 2017 baada ya kunaswa wakishiriki vitendo vya ushirikina. Waumini wetu wengi wamekiri waziwazi kwamba, wanajihusisha na ushirikina ili kujipa ahueni ya kimaisha,” Amasema Askofu Mburu. Kongamano hilo ambalo linamalizika leo Jumanne limetuma ujumbe kwa ofisi za serikali, mabunge na asasi nyingine kwamba ndani ya idara hizo kunashuhudiwa kiwango kikubwa cha uchawi na ushirikina. Kwa upande wake Padri Joseph Wamalwa wa Kanisa Katoliki Kaunti ya Nairobi amesema kuwa ongezeko la ushirikina na uchawi miongoni mwa Wakenya linadhihirika kutokana na visa mbalimbali vinavyoshuhudiwa kila mara ikiwemo vitendo vya kulishwa nyasi, matukio ya unyofoaji kiholela wa sehemu za siri na pia mauaji ya walemavu wa ngozi (Zeruzeru), huku Wakristo wengi wakinaswa wakiwa wamevaa hirizi mwilini kwa dhana ya kujikinga na mikosi ya kijamii, kiuchumi au kisiasa.
Sehemu ya uchawi 
Padri Wamalwa amefafanua zaidi kwa kusema, mwaka jana  Shirika la The Pew Research Centre la nchini Marekani lilitoa ripoti ikionyesha kuwa, Wakenya wengi bado wanaabudu miungu ya jadi, kutoa kafara, kujihusisha na ushirikina mbalimbali sambamba na kuamini mapepo ya kuzimu. Amesema: “Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Kenya iko mbele kuliko nchi kama Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Ethiopia, Nigeria, Zambia na Rwanda katika kuamini ushirikina na uchawi.” Pia amesema, asilimia kubwa ya Wakristo na Wakenya waliohojiwa wamekiri kuvaa hirizi na pia kwenda kwa waganga wa kienyeji.
CHANZO:-http://parstoday.com/sw/news/africa

Monday, March 19, 2018

PICHA:- JINSI ILIVYOFANA HAFLA YA KUTUNUKU VYETI VYA TUZO ZA MWANAMKE JEMBE 2018.

Mkuu wa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza Mhe. Marry Tesha akihutubia kusanyiko la utoaji wa Vyeti vya Tuzo za Mwanamke Jembe zilizoandaliwa na kituo cha redio Jembe Fm kutoka Mwanza, hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki Jembe Beach jijini humo.
Serikali inatambua na kuthamini sana ushirikiano baina yenu na harakati za maendeleo katika Mkoa wetu.  

Ndiyo maana tumekuwa tunatengeneza mazingira mazuri kwa wanawake. Tumekuwa tunatoa mikopo kwa makundi ya wajasiriamali tumewaboreshea vituo Afya ,na mazingira mengine mengi.
Meneja wa Jembe Media Group Fred Kikoti akitoa historia ya kituo na shughuli mbalimbali za kituo kwa jamii tangu uanzishwaji wake.
Wadada makini wa Mwanza ndani ya  kusanyiko.
Sehemu ya wahudhuriaji wa hafla ya Mwanamke Jembe.
Safi.
Tunaimani mchakato huu ulifuata hatua zote stahiki za kumpata Mwanamke Jembe ambaye anawakilisha  WANAWAKE  MAJEMBE wengine kutoka katika mkoa wetu, hii ni hatua nzuri ya kuwainua wanawake hawa ili na wao wafike katika  viwango vinavyohitajika katika soko la sasa la kimapinduzi katika maendeleo.
Kwa umakini wadau wakifuatilia kilichokuwa kikijili wakati huo.
Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la KIVULINI Bw. Yassin Ally amesema wanawake wengi huangushwa na wanawake wenzao.
Mmoja kati ya wafanyabiashara wenye mafanikio jijini Mwanza Dida Vitenge Wear naye alisimama kutoa neno la shukurani sanjari na kuwasilisha uzoefu alioupata kupitia harakati zake za ujasiliamali.
Team Sega "Mambo ni Motto" nao walishiriki kama wadhamini Mwanamke Jembe 2018.
Aksante sana kwa Lake Zone Tents and Supply kupitia Bi. Rose kwa kuwa sehemu ya wadhamini wa Mwanamke Jembe 2018.
Meneja wa Vipindi kituo cha Redio Jembe Fm Kelvin Michael (Deejay Kflip) akitambulisha safu ya watangazaji wa Jembe Fm (hawapo pichani).
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza Mhe. Marry Tesha akimpongeza mshindi wa kwanza Tuzo za Mwanamke Jembe 2018 Bi. Amina Khamisi ambaye amekuwa akiishi na virusi vya ukimwi tangu mwaka 1982 na amekuwa akiwahudumia na kuwapa moyo na darasa la masuala ya afya watu waishio na VVU, ni kupitia tuzo zilizoandaliwa na kituo cha redio Jembe Fm Mwanza, hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki Jembe Beach jijini humo.
Dada huyu (kulia) Deborah Mwambo ni mjasiliamali licha ya kukosa ada akiwa hana wazazi wa kumsaidia aliamua kujishughulisha na kazi za ndani huku akijisomesha leo hii anajivunia mafanikio aliyonayo kwani ameweza kujenga nyumba pia akijitegemea. 
Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la KIVULINI Bw. Yassin Ally (kulia) akikabidhi Bi. Aisha Mtumwa Cheti cha Tuzo ya Huduma kwa Watoto.
Mkurugenzi wa Club 255 Bi. Siwema (kushoto) akimkabidhi Cheti cha Tuzo za Mwanamke Jembe kipengele cha Michezo iliyokwenda kwa Consolata Lazaro (kulia) ambaye ni mwamuzi wa kike wa Ligi kuu Soka Tanzania Bara kutoka Mwanza. 
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza Mhe. Marry Tesha (kulia) akikambidhi cheti cha Shukurani kwa Meneja wa Jembe Media Group Fred Kikoti na hii ni kwa niaba ya kutambua mchango wa Mkurugenzi wake Dr. sebastian Ndege kwa shughuli na harakati za akinamama mkoa wa Mwanza katika hafla ya Tuzo za Mwanamke Jembe zilizofanyika mwishoni mwa wiki.
Mkuu wa Vipindi toka Jembe Fm Radio Kelvin Michael (kushoto) akimkabidhi Cheti cha Shukurani na kutambua mchango wa Mkuu wa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza Mhe. Marry Tesha katika hafla ya kukabidhi Tuzo za Mwanamke Jembe zilizofanyika mwishoni mwa wiki jijini Mwanza.
 Aksante ni neno kubwa sana.
Mkuu wa Vipindi Msaidizi wa Jembe Fm Radio Harith Jaha (kulia) ambaye alikuwa Jaji Mkuu wa mchakato mzima, akifafanua sifa za mshiriki mshindi wa Kwanza Amina Khamisi kabla ya kumkabidhi Tuzo na Cheti katika hafla ya kukabidhi Tuzo za Mwanamke Jembe zilizofanyika mwishoni mwa wiki jijini Mwanza.
Ilivyokuwa Jiografia ya eneo la tukio.
Mwanamke Jembe.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Marry Tesha akikata keki iliyoandaliwa kama sehemu ya kumbukumbu ya maadhimisho ya Tuzo za Mwanamke Jembe 2018.
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza Mhe. Marry Tesha katika picha ya pamoja wadau wafanikishaji kutoka kushoto Meneja wa Jembe Media Group Fred Kikoti, Mratibu wa Mwanamke Jembe 2018 Mansour Jumanne na Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la KIVULINI Bw. Yassin Ally (kulia)
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza Mhe. Marry Tesha katika picha ya pamoja na Ma-Mc wa tuzo sanjari na wadau wa Meza kuu. 
Picha ya pamoja.
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza Mhe. Marry Tesha katika picha ya pamoja na washiriki wa Tuzo sanjari na wadau wa Meza kuu.
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza Mhe. Marry Tesha katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Jembe Fm Mwanza.

HOTUBA YA MKUU WA  MKOA WA MWANZA  , MHESHIMIWA   JOHN MONGELA  AMBAYO ITASOMWA NA MKUU WA WILAYA NYAMAGANA MAMA MARRY TESHA , KATIKA UTOAJI WA VYETI NA ZAWADI KWENYE KILELE CHA  MWANAMKE  JEMBE  MWANZA , TAREHE 17  MARCH , 2018

Waheshimiwa viongozi wa JEMBE MEDIA GROUP,

Waheshimiwa Wageni Wote toka Ndani na Nje ya Mkoa wa Mwanza;
Waheshimiwa Wanawake Wote Mliopo Hapa;
Mkurugenzi wa Kivulini Bw. Yassin Ally;
Mabibi na Mabwana;
Bwana Yesu Asifiwe : AsalamAleikum
Mwanamke JEMBE Oyeee
Mwanamke Jembe Saaafiiii

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya njema katika siku ya leo, Pia napenda kuwashukuru sana Uongozi wa Jembe Fm kwa kunialika na kunishirikisha kwenye ugawaji wa vyeti kwa akinamama, wadada ambao wamekuwa sehemu ya maendeleo ya jamii yetu, na sehemu ya maendeleo katika mkoa wetu wa Mwanza  yaani (MWANAMKE JEMBE) Kwa kweli ni jambo la furaha na heshima kubwa kwangu kujumuika nanyi kwa tukio hili kubwa na la kihistoria katika Mkoa wetu.

Mwaliko wenu huu kwangu ni uthibitisho mkubwa wa uhusiano mzuri uliopo baina ya JEMBE FM 93.7 MWANZA, Wakina Mama  na Serikali Katika Mkoa wetu.

Uhusiano ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa mkoa wetu na watu wake. Uhusiano  ambao umejitafsiri katika umoja, upendo, amani, na mshikamano uliopo baina ya WanaMwanza

Mwanamke Jembe
Ndugu wanawake, Wananchi na Wageni Waalikwa;

Miaka 5 iliyopita, Mkurugenzi wa kituo cha Radio Jembe fm, DR. Sebastian Ndege  alikuja na wazo la kuanzisha kituo cha radio Mkoani Mwanza wazo lake lilifanikiwa na ndipo hapo kituo cha Radio cha Jembe Fm kikaanzishwa katika mkoa wetu wa Mwanza, Kituo hiki kilianzishwa Kwa lengo la kuwa habarisha wana Mwanza, kuburudisha na kuelimisha, Pamoja na yote hayo kituo cha radio Cha jembe FM, kimekuwa sehemu ya msaada kwa wananchi na kimekuwa kiunganishi kati yetu na jamii.

Huo pia ndiyo misingi wa JEMBE fm ambayo imekuwa tegemeo kubwa kwa Wananchi wa MWANZA.

Licha ya kutumia viongozi wetu wa mitaa wakiwemo wenyeviti na mabalozi, katika ufikishaji wa taarifa na elimu kwa wananchi, SISI Serikali Jitihada zetu za kuondoa umasikini, kuboresha huduma za afya na masuala mengine muhimu kwa miaka ya sasa yenye mapinduzi ya teknolojia hutegemea kwa namna kubwa sana uwepo wa vyombo vya habari.

Jitihada za Serikali zinapounganika na zile za vyombo vya habari tunatengeza nguvu kubwa ya kuwaondolea wananchi wetu siyo tu unyonge wa kukosa habari, bali pia kuwapunguzia changamoto za maendeleo zinazowakabili na kusaidia kuinua hali zao za maisha.

Mchango wa Jembe FM katika Mkoa wetu
ndugu Wanawake .

Ninaposema hivyo, natambua mchango wa Jembe FM katika kuhabarisha jamii ya watanzania hususani mkoa wetu wa Mwanza, Mimi ni shahidi, maana nimekuwa nikipata taarifa ya habari kutoka katika kituo hiki cha habari, nimewahi kuwa shuhudia Jembe fm katika Kampeni ya Usalama barabarani ambayo walishiriki bega kwa bega na jeshi letu la Polisi kitengo cha Usalama barabarani.

Nimeshuhudia Jembe Fm wakiwa na kampeni ya kumwinua mtoto (MTOTO JEMBE) Pia hata katika burudani wote tumekuwa tukishuhudia Jembe Fm wa kituletea wasanii kutoka ndani na nje ya Tanzania  kupitia Tamasha lao la kila mwaka la JEMBEKA FESTIVAL, Tuliwahi kuwashudia hata wasanii wa kimataifa, kutoka nchini Marekani akina NEYO na wengine wengi na hata wale wanaotamba hapa nchini  akina Diamond,Maua Sama, Juma Nature, Ruby nakadhalika. Tena mwaka huu tamasha hilo sijaliona sijui kwanini?

JEMBE FM  inatoa habari za kipekee ambazo hazipatikani kwa urahisi katika vituo vingine vya habari.

Ninyi mna vipindi vizuri kama : KAZI NA NGOMA , DRIVE MIX, SEGA LA LEO, MCHAKAMCHAKA, KIKOBA, SPORTS RIPOTI  NK , Hivi tu ni baadhi ya vipindi ambavyo kwetu tunadiriki kusema kuwa mnafanya kazi nzuri.

Kwa upande wa Afya nimekuwa nikiwasikia namna mnavyo hamasisha watu kuwasaidia wenye matatizo ya Afya na saa nyingine kuhamasisha watu kuwachangia ili wafanikishe ndoto zao, Hongereni sana.

Kwa miaka mingi sana wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki zao za msingi na kupigania maendeleo si tu ya jamii inayowazunguka bali hata kwa maendeleo ya taifa na mtu mmoja mmoja, Niwapongeze wanawake wote  wa mkoa wa Mwanza kwa kulifanikisha hilo.

Miaka ya zamani wanawake walikatazwa kujishughulisha na shughuli za uzalishaji na kiuchumi na walikuwa ni watu wa ndani tu, ila tunaishukuru jamii kwa kutambua umuhimu wa wanawake na kuwaruhusu kuingia katika shughuli za uchumi, na uzalishaji mali, na ndio maana leo tunashuhudia idadi kubwa ya wajasiriamali, wafanyabiashara wakubwa, madaktari, wahandisi, waandishi wa habari, walimu na wanajamii wakutosha ndani ya mkoa wetu.

Mwanamke Jembe mlianza rasmi mwaka Jana, mwaka huu naona mmeboresha zaidi lakini tunawaomba mwakani mwanamke  JEMBE iwe maradufu zaidi ya hii ya leo, kuwe na zawadi za kutosha, wadhamini wajitokeze kuwasapoti na sisi Serikali tunawaahidi hatutawaangusha, na hiki mlichokifanya leo ni wazi kuwa mnafanya kazi nzuri sana.

Tunaimani mchakato huu ulifuata hatua zote stahiki za kumpata Mwanamke Jembe ambaye anawakilisha  WANAWAKE  MAJEMBE wengine kutoka katika mkoa wetu, hii ni hatua nzuri ya kuwainua wanawake hawa ili na wao wafike katika  viwango vinavyohitajika katika soko la sasa la kimapinduzi katika maendeleo.

Tunawashukuru wadau wote walioshirikiana na Jembe fm katika kuifanikisha hili, Wakina mama walijitokeza hapa, wakina mama ambao wamekuwa wakijituma na kupambana katika Nyanja tofautitofauti , marafiki wote mliokuja kushuhudia utoaji wa vyeti, Tunawashukuru sana.

Na pia napenda kupitia hafla hii kuwashukuru ninyi Jembe fm, Mkurugenzi Dr Sebastian Ndege, Meneja Fred Kikoti, Mkuu wa vipindi, Kelvin Michael, Mratibu wa Mwanamke Jembe Mansour Juamnne, viongozi na watangazaji wote kwa kazi yenu nzuri mnayoifanya.

Vile vile, nawashukuru sana kwa kuiungamkono Serikali ya Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli katika jitihada za kuwaletea maendeleo Watanzania.

Nawaomba muendelee na moyo huo mwema. Namuomba Mwenyezi Mungu awaongezee pale mlipopunguza na kuendelea kuwashushia Baraka tele.

Wanawake Oyee

Serikali inatambua na kuthamini sana ushirikiano baina yenu na harakati za maendeleo katika Mkoa wetu.  

Ndiyo maana tumekuwa tunatengeneza mazingira mazuri kwa wanawake. Tumekuwa tunatoa mikopo kwa makundi ya wajasiriamali tumewaboreshea vituo Afya ,na mazingira mengine mengi
Asanteni sana kwa kunisikiliza.