ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, September 28, 2016

WAZIRI MAJALIWA AKUTANA NA WAWEKEZAJI KUTOKA KOREA YA KUSINI.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa makampuni mbalimbali kutoka Korea ya Kusini ambao wamekuja Tanzania kuona fursa mbalimbali za uwekezaji. Mazungumzo hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam  Septemba 27, 2016. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika  picha ya pamoja na  viongozi wa makampuni mbalimbali ya Korea Kusini ambao wapo nchini kuona fursa  mbalimbali za uwekezaji  nchini. Picha hiyo ilitanguliwa na mazungumzo yaliyofanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Septemba 27. Watatu kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Angelina Mbula.


 Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa akikabidhiwa jezi yanye maneno  Hapa Kazi Tu  iliyotolewa na wawekezaji kutoka Korea ya Kusini waliokuja nchini kuona fursa mbalimbali za uwekezaji.  Awali Waziri Mkuu alizungumza na wawekezaji hao ofisini kwake jijini Dar es salaam Septemba 27, 2016. Kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula. 
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na wawekezaji wa kampuni tisa za nchini Korea Kusini  na kumuahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuwekeza katika sekta ya kilimo, viwanda, maji, miundombinu, elimu, afya na michezo.

Wawekezaji hao wanatoka kampuni ya Sima textile, ESM, Jusung Solar Engineering, Seongnam City FC, Yeong Yang City Korea,Ulsan Vocational Training, Egis Smart City, MBN

Akizungumza na wawekezaji hao jana jioni (Jumanne, Septemba 27, 2016) kwa niaba ya Mhe. Rais Dk. John Magufuli, Waziri Mkuu alisema kwamba Tanzania ni sehemu salama kwa uwekezaji ikiwa na fursa za uwekezaji kwenye sekta nyingi kama miundombinu, kilimo na viwanda. Licha ya mazingira mazuri ya uwekezaji pia aliwahahakishia ulinzi kwenye uwekezaji wao.

Waziri Mkuu alisema Korea ya Kusini inashirikiana vizuri na Tanzania hivyo wanatarajia mengi kutoka nchini huko kupitia wawekezaji hao.

Wawekezaji hao tayari wamefanya mazungumzo na viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijinii Mwanza na kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya miradi minne ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya maji, kiwanda cha nguo, zana kubwa za kilimo na mafunzo ya ufundi.

Kwa upande wake Mkuu wa Msafara huo, Bw. Son Young Soo alisema amefurahishwa na ziara waliyofanya nchini na wapo tayari kuwekeza  nchini.

Naye, Bw. Jihyun Kim wa  kampuni ya Yeong Yang City Korea ambayo inashughulikia masuala ya kilimo cha mbogamboga alisema watawekeza kwenye kilimo  hususan cha zao la pilipili na watajenga kiwanda kwa ajili ya usindikaji.

Naye Mkurugenzi wa Klabu ya Soka ya Seongnam Bw. Suk Hoon Lee alisema klabu yake ipo tayari kuwekeza katika shule ya michezo kwa vijana ili kuongeza kasi ya maendeleo ya soka.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.